ila ninapotafakari kuhusu shukrani huwa nakumbuka kisa cha
zamani cha simba aliyejeruhiwa. Kulikuwa na mzee aliyejenga
nyumba yake katikati ya msitu. Siku moja jioni alikuwa ameketi
upenuni mwa nyumba yake akichonga mpini wa jembe. Mara
akashtuka alipoona kitu kizito kimetua begani kwake na
kuning’inia mbele ya kifua chake. Kwa mshangao mkubwa
akagundua kuwa ulikuwa mguu wa simba. Ulikuwa unavuja
damu nyingi kwa kuwa ulikuwa umechomwa na kipande cha mti
chenye ncha kali.
Mzee aliingiwa na woga mkubwa akataka kukimbia lakini
akamwonea huruma yule simba. Akaushika ule mguu na
kuchomoa kile kipande cha mti. Simba aliposaidiwa akamtazama
yule mzee kwa muda na kuondoka akielekea msituni. Baada ya
siku chache simba alirejea nyumbani kwa mzee huku akiwa
amebeba swala mkubwa. Alipofika akamtazama yule mzee usoni,
akamtua yule swala, akafanya ishara fulani na kuondoka
akirejea msituni. Mzee akabaki ameduwaa kwa kuona jinsi
simba alivyomshukuru kwa kumletea zawadi.
Kisa hiki kinatuonyesha tabia ya shukrani ambayo ni wajibu
kwa viumbe wote. Tangu binadamu anapozaliwa hadi
anapozeeka maisha yake hupitia katika mikono ya watu wengi.
Hakuna mtu anayeweza kujilea na kujiendeleza yeye mwenyewe
hadi anapozeeka. Maisha yetu na maendeleo yetu yote
hutegemea watu wengine.
Jinsi unavyoonekana leo na hatua uliyofikia kuna watu wengi
waliokufikisha hapo ulipo. Kuna wazazi wako, walimu, majirani,
marafiki, ndugu na jamaa zako na jamii inayokuzunguka kwa
ujumla. Juu ya wote kuna Mwenyezi Mungu aliye mkuu kuliko
wote. Yeye ndiye aliyetuumba sisi wote, ulimwengu wetu na
vyote vilivyomo ndani yake.
Baada ya haya yote naona nikuulize swali. Je, baada ya Mungu
aliyekuumba na matendo uliyotendewa na wazazi na walimu
wako, kuna matendo mengine yoyote uliyotendewa na watu
wengine ambayo yameleta maendeleo katika maisha yako? Je,
unaweza kuorodhesha watu waliokutendea mambo hayo na
manufaa au mabadiliko ambayo mambo hayo yamekuletea katika
maisha yako?
Duniani tunatendewa mambo mengi mazuri na watu tunaoishi
nao, tunaokaa nao kwa muda fulani na hata wale tunaokutana
nao mara moja tu hata kwenye foleni au tukiwa katika vyombo
vya usafiri. Wakati mwingine unaweza kufikiria ni tendo dogo tu
lakini hatimaye likawa na manufaa makubwa sana katika
maisha yako yote.
Nakumbuka kisa cha kijana aliyekuwa akilala barabarani na
kuokota chakula kwenye mapipa ya taka. Siku moja mtu mmoja
mkarimu akamwonea huruma akamuokota na kumpatia kazi ya
kuuza magazeti mitaani. Aliifanya kazi hiyo kwa bidii, juhudi na
maarifa. Baada ya miaka michache aliamua kuanzisha gazeti lake
la kila siku. Gazeti hili likatokea kuwa maarufu sana nchini
kwake. Je mtu aliyemtendea kijana huyo kitendo cha kumsaidia
akamtoa katika hali ya kulala jalalani hadi kuwa milionea
anastahili kushukuriwa vipi?
Kila tunaposikia mambo wanayotendewa watu hadi wakapata
mafanikio ya pekee kama yaliyosimuliwa katika kisa hiki,
tunapata hisia kuwa hatuna budi kuwathamini na kuwashukuru
waliotutendea mambo mema katika maisha yetu. Hii haijalishi
kama jambo tulilotendewa ni dogo au kubwa. Kitu cha msingi ni
ile dhamira anayoweka mtu katika nafsi yake hadi akakutendea
jambo hilo. Hii ndiyo tunayopaswa kuishukuru.
Katika baadhi ya nchi tabia ya kushukuru hata katika mambo
madogo huthaminiwa sana hadi imekuwa sehemu ya utamaduni
wao. Mathalani wao humshukuru na kumpa bahashishi hata
mtumishi aliyewahudumia katika mkahawa ambaye ameajiriwa
kufanya kazi hiyo. Hata wanapokodisha teksi humshukuru na
kumpa bahashishi dereva atakapopakia au kuteremsha mizigo
katika gari waliyoikodisha.
Shukurani sio lazima iwe zawadi kama vile fedha au vitu
vingine. Kufanya kitendo chochote cha kumwonyesha
aliyekutendea wema au hisani kuwa amekufurahisha kinatosha
kuwa shukurani. Kwa mfano, kijana anapokupisha kwenye kiti
kwenye basi unaweza kumshukuru hata kwa neno “asante” au
tabasamu tu.
Shukurani ni tabia ya kiungwana. Hebu soma kisa hiki.
Kulikuwa na msichana kipofu ambaye hakufurahia kitu chochote
katika maisha yake isipokuwa kijana mmoja
Comments
Post a Comment